CAG yabaini madudu katika halmashauri ya jiji la Tanga


TANGA
Kamati ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa nchini imebaini uwepo wa madudu mengi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya halmashauri ya jiji la TANGA huku kamati hiyo ikitoa  maagizo mazito kwa halmashauri ya jiji la Tanga.

Miongoni mwa madudu hayo ni uwepo wa suala la ukosefu wa uratibu,uandaaji sanjari na usimamizi bora wa miradi ya halmashauri kwa muda mrefu.

Nyengine ni kutokua na ushirikishwaji wa vijana katika utekelezaji wa miradi mingi ya uwekezaji jambo ambalo linawanyima fursa vijana ya kutambua fursa za kazi zitokanazo na uwekezaji husika katika halmashauri hiyo.
Hayo yamebainika katika ziara ya kamati hiyo walioifanya jijini Tanga juu ya kuitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo mbele ya waandishi wa habari,viongozi wa halmashauri ya jiji,viongozi wa wilaya sanjari na mkoa kwa ujumla,Mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimiwa ABDALLAH CHIKOTA amesema mbali na kubaini hayo pia wamebaini uwepo wa taarifa zinazokinzana za watendaji wa halmashauri juu ya utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo katika halmashauri hiyo.

Mhe.Chikota amesema miongoni mwa miradi walioigundua uwepo wa kasoro hizo ni mradi wa maji katika kijiji cha mwarongo kata ya MARUNGU uliogharimu shilingi milioni 622.9 ambao umekua ukisuaua kuwahudumia wananchi wa maeneo husika kutokana na kupasuka kwa mabomba ya mradi huo.

Mradi mwengine ni ule wa milioni 280.6 wa soko la mgandini liliopo kata ya MWANZANGE ambao umegubikwa na dosari lukuki ikiwa ubovu wa miundombinu ya soko, ukosefu wa uzio,maji,umeme ,baadhi ya maeneo ya soko kuvuja sanjari na ukosefu wa hali ya ushirikishwaji na mawasiliano mazuri kati ya wafanyabiashara wa soko hilo na uongozi wa halmashauri jambo ambalo huleta mgongano wa mara kwa mara baina yao.

Katika hatua nyengine mwenyekiti huyo ametoa maagizo ya kamati hiyo ambapo imeuagiza uongozi wa halamashauri hiyo kutekeleza kwa vitendo suala la kisheria ya kutoa asilimia kumi ya vijana na wakinamama katika halmashauri hiyo kwa kuwa kumebainika sheria hiyo haifuatwi ipasavyo katika halmashauri hiyo.

Halikadhalika kamati hiyo imepiga mafuruku tabia ya viongozi wa halmashauri hiyo kuingia mikataba ambayo haina masilahi katika taifa kwa kuwakodisha wawekezaji  ardhi na huku kamati hiyo ikiiagiza halmashauri ya jiji kutoingia mkataba wa aina yeyote ile na wawekezaji hadi jopo la viongozi wa mkoa,wizara husika itakapo kaa na kujiridhisha kuhusu tija ya mkataba husika katika halmashauri.

Pia kamati imeuagiza uongozi wa halmashauri ya jiji la Tanga kuzifanyia utatuzi changamoto zote zilizobainika katika miradi hiyo ambapo hadi ifikapo April 28 mwaka huu taarifa ya utekelezaji wake iwe imekwishawasilishwa katika ofisi za CAG na nakala ipelekwe katika kamati hiyo.

Kwa upande wao katibu tawala mkoa wa Tanga,Mhandisi.ZENA SAID,mkuu wa wilaya ya Tanga,THOBIAS MWILAPWA,Mstahiki meya wa jiji la TANGA Mhe.SELEBOSS MUSTAPH MHINA pamoja na  mkurugenzi wa jiji la Tanga DAUDI MAYEJI,wameipongeza kamati hiyo kwa ziara walioifanya na huku wakiahidi kutekeleza agizo hilo mapema iwezekanavyo.



No comments