Milioni 60 kumwagwa korogwe mji.

KOROGWE .

Halmashauri ya MJI KOROGWE mkoani TANGA,imedhamiria kutoa shilingi milioni 60 kwa wananchi wa halmashauri hiyo ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza na MAJLISI MEDIA hii leo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Ndugu.JUMANNE SHAURI amesema fedha hizo wazitarajia kuzitoa ndani ya mwaka huu 2018 ambapo ni mwendelezo wa utoaji wa asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya vijana na wakinamama.

Aidha,amesema kwa kipindi cha mwaka jana pekee walitoa shilingi milioni 40 kwa walengwa hao na sasa wanajishughulisha  katika vikundi hai vya ujasiriamali na biashara ndogo ndogo ikiwemo utengenezaji wa viatu sambamba na kujishughulisha na usafiri wa bodaboda.

Mkurugenzi huyo amesema walengwa hao wanawezeshwa nyenzo za biashara na si pesa tasilimu kama watu wengine wanavyodhani na tayari jopo la wataalumu wa ujasiriamali kutoka SIDO,maafisa ugavi na maafisa biashara wanaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa walengwa ili waweze kuisimamia mitaji yao vizuri.

Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali walionufaika na asilimia hiyo mwaka jana wameipongeza halmashauri hiyo kwa kuwakumbuka na kuahidi kuitumia kwa matumizi chanya mitaji mingine watakayopatiwa mwaka huu.

Katika hatua nyengine mkurugenzi JUMANNE SHAURI ameizungumzia mipango mikakati walionayo katika halmashauri ni ujenzi wa soko kubwa la kisasa katika halmashauri ambapo ujenzi huo unatarajia kuaanza mwezi wa pili mwaka huu,ujenzi wa Viwanda vidogo vidogo ikiwemo kiwanda cha viatu,mkonge,kujenga kiwanda cha usindikaji matunda katika halmashauri na pia tayari wametenga zaidi ya ekari 4000 kwaajili ya wawekezaji mbalimbali katika halmashauri.

Awali amelizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ambapo amesema asilimia 30 ya mapato ya halmshauri hutokana na stendi mpya ya kisasa iliopo katika halmashauri hiyo ambayo kwa siku hukusanya zaidi ya milioni moja.

Halikadhalika amewaomba wananchi wa halmashauri hiyo kuwa na mwitikio katika suala la kuitumia stendi hiyo ili kuiwezesha halmashauri iweze kufanikisha adhima ya serekali ya kufikia uchumi wa kati katika suala la ukusanyaji wa mapato ambapo amesema kuna baadhi ya wananchi hawaitumii ipasavyo stend hiyo na kusubiri usafiri barabarani jambo ambalo amesema linarudisha nyuma jitihada za ukusanyaji wa mapato kwa wingi katika stend hiyo.




No comments