Walichokibaini Polisi baada ya kumhoji 'Nabii' Tito
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, linamshikilia Tito Onesmo Machibya anayejulikana kama ‘Nabii’ Tito (44) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nong’ona Manispaa ya Dodoma, kwa kosa la kueneza chuki ya kidini dhidi ya watu wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumanne, Januari 22, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Muroto, amesema kuwa ‘Nabii’ Tito amekamatwa baada ya kurekodi vipande vifupi vya video na picha vyenye maudhui ya kukashifu dini nyingine, na kuleta chuki dhidi ya watu wengine na kurusha katika mitandao ya kijamii pamoja na kusambaza vipeperushi kinyume na kifungu cha sheria namba 129 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 na marekebisho yake ya 2002.
“Tafasiri ambazo amekuwa akizitoa ni za upotoshaji na amekuwa akifanya vitendo vya udhalilishaji hadharani na kuchochea maovu kwa jamii” amesema Kamanda Muroto.
Nabii Tito amekamatwa akiwa na majoho (kanzu) mawili yakiwa na misalaba miwili, vipeperushi 80, CD pamoja na Biblia moja, vitu ambayo amekuwa akivitumia katika mafundisho yake.
Aidha Kamanda Muroto ameeleza kuwa kwa Machibya ameonekana kuwa na historia ya kichaa na amewahi kufikishwa katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam na Hospitali ya Mirembe ambako kote madaktari hao walithibitisha kuwa ana ugonjwa wa akili.
“Katika Uchunguzi wa awali, Tito Onesmo Machibya ‘Nabii Tito’ ameonekana kama ana historia ya kichaa, kwa mujibu wa taarifa za madaktari,” amesema kamanda Muroto. Hata hivyo Jeshi la polisi bado linamshikilia Nabii huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi pamoja na usalama wake, huku wakiendelea kuwatafuta watu anaoshirikiana nao katika kueneza mafundisho hayo yenye kupotosha, na atakapopatikana na hatia atachukuliwa hatua zaidi za kisheria.
Post a Comment