Zanzibar yakabiliwa na upungufu wa madaktari Bingwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekjiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohammed Shein amesema upungufu wa Madaktari bingwa na wataalamu wa fani ya afya unaathiri utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi visiwani Zanzibar.
Aidha Rais Shein amesisitiza kuwa Serikali yake kuanzia Mwezi Julai mwaka huu itarejesha utaratibu wa elimu bure kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.
Dkt. Shein ameyasema hayo leo katika sherehe za Kilele cha Maadhimisho ya 54 ya Mapinduzi ya Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja wa Amani mjini, Unguja.
Katika Sherehe hizo maelfu ya wananchi walijitokeza wakiwemo na viongozi wakuu wa nchi, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, pamoja na viongozi wengine wa Bara na visiwani.
Aidha Dkt. Shein amesisitiza kuwa serikali yake inazitambua changamoto zote za masuala ya afya na kuahidi kuyatatua likiwemo la madaktari, vifaatiba pamoja na miundombinu.
Katika hatua nyingine Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein amewatunuku nishani za heshima viongozi na watumishi wa umma 43 katika maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Waliofanikiwa kutwaa nishani hizo ni pamoja na waasisi, washiriki na wote walioyaenzi Mapinduzi ya Matukufu ya Zanzibar yaliyotokea mwaka 1964.
Pamoja na hayo, Dkt. Shein amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo ili kuwa chachu ya kuendelea kuwa kivutio kikubwa kwa uwekezaji miradi mikubwa ya maendeleo .
Sanjari na maadhimisho hayo mbali na kutunuku nishani hizo, Serikali ya Zanzibar imezindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni ishara ya ukombozi wa fikra na maendeleo ya kiuchumi wa taifa hilo.
Post a Comment