Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kurudisha fedha kwa Mwalimu
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema
itarejesha kiasi cha shilingi 282,000 ilizomkata kimakosa Mwalimu Edwini
Ndyamukama wa jijini Mwanza baada ya kugundua Mwalimu huyo hadaiwi na Bodi
hiyo.
Taaarifa iliyotolwa na Bodi ya Mikopo inaeleza kuwa kanzidata ya
Bodi ya Mikopo haimuoneshi Mwalimu Edwini Ndyamukama kama mdaiwa na baada ya
uchunguzi imebainika kuwa anayedaiwa na Bodi hiyo ni Edwin F. Ndyamukama aliyesoma
Chuo Kikuu Kishiriki cha Archbishop James (AJUCO) ambaye alikopeshwa na kupokea
zaidi ya Shilingi milioni 2.29 hadi kufikia mwaka 2015.
“Ni kweli Mwalimu Ndyamukama mwenye namba ya mtihani wa Kidato
cha nne S0304.1993 anadai kurejeshewa shilingi 282,000 alizokatwa kama
marejesho ya mkopo wa elimu ya juu. Malipo haya na mengine yanakamilishwa na
yatawekwa katika akaunti yake ya benki kabla ya Jumanne wiki ijayo,” inaeleza
taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa malipo hayo yanafanyika baada ya kukamilika
kwa ukaguzi na uchunguzi uliothibitisha kuwa malalamikaji hakunufaika na fedha
za mkopo na kwamba hao ni watu wawili tofauti.
“Ni vema kufahamu kuwa makato katika mshahara wa Mwalimu Edwini
ambaye ni mlalamikaji yalisitishwa na alipewa taarifa, lakini kilichokuwa
kinafanywa na Bodi ni kuondoa shaka ya yeye kuwa si mnufaika wa mkopo kwani
kumekuwa na matukio ya watu kulalamika lakini baada ya uchunguzi inagundulika
kuwa wengine ni wadaiwa,” inafafanua taarifa hiyo.
Katika malamiko yake, Mwalimu Edwini Ndyamukama alinukuliwa na
Gazeti la Uhuru la Januari 3 mwaka huu akieleza kuwa Bodi ya Mikopo walimkata
fedha katika mshahara wake wa mwezi May na June mwaka jana wakati yeye hakuwahi
kukopeshwa na Bodi hiyo.
Mwalimu Edwini alieleza kuwa baada kuona amekatwa fedha
aliandika barua ya malalamiko na Bodi walisitisha kukata mshahara wake lakini
alikuwa bado hajalipwa fedha zilizokatwa kimakosa.
Post a Comment