Mapato ya Korosho 2017/18 kwa mikoa minne yafikia trilioni 1.08



medaiwa kua mapato ya yaliyotokana na mauzo ya korosho katika msimu wa 2017/18 katika mikoa minne ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma yamepanda na kufikia shilingi trilioni 1.08 ikilinganishwa na misimu miwili iliyopita.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Hassan Jarufu ametoa taarifa hiyo jana Jumapili, Desemba 31, wakati akitoa ufafanuzi juu ya uzalishaji wa zao korosho nchini.

“Ukiangalia msimu wa mwaka 2015/16, utaona kuwa korosho zilizozalishwa zilikuwa kidogo zaidi. Msimu huo ziliuzwa kilo 155,244,645 zikiwa na thamani ya shilingi bilioni 3.88 ikilinganisha na msimu wa 2016/17 ambapo jumla ya kilo 265,237,845.00 ziliuzwa zikiwa na thamani ya shilingi bilioni 8.71,” alisema.

Alisema katika minada 10 ya msimu wa 2017/18, mauzo ya korosho yamefikia kilo 285,828,205 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.08. “Mnada wa 10 ulikuwa tarehe 21 Desemba, 2017 na minada bado inaendelea kwa msimu wa  2017/2018,” alisema.

Akitoa ufafanuzi wa mauzo hayo kwa mikoa hadi kufikia mnada wa 10, Jarufu alisema Mkoa wa Mtwara umeongoza kwa kuuza tani 178,165.741 zenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 701 ukifuatiwa na Mkoa wa Lindi ambao umeuza tani 68,687.504 zenye thamani ya shilingi milioni 247.

“Mkoa wa Ruvuma umeuza tani 19,545.613 zenye thamani ya shilingi 76,173,400,063.00 na Mkoa wa Pwani umeuza tani 19,429.347 zenye thamani ya shilingi 57,189,224,856.00 na kufanya mapato yote kwa mwaka huu kufikia shilingi trilioni 1.082,” alisema.

Jarufu alitoa ufafanuzi huo mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 kwa msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.

No comments