Sababu za kutofikia malengo kwa shule za kiislamu TANGA zatajwa.
Imeelezwa kuwa ukosefu wa
mikataba ya kazi kwa walimu,kutothaminiwa,kulipwa ujira mdogo sambamba na
kutopatiwa mishahara kwa wakati zimetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu
zinazosababisha kutofikia malengo kwa baadhi ya shule za kiislamu mkoani TANGA.
Hayo yamebainishwa hii leo
na KHATWIBU SIRAJ MAGAYANE ambae ni
mwanataaluma ya ualimu katika shule za kiislamu mkoani hapa wakati alipokua
akifanyiwa mahujiano mahsusi na mwanahabari wa MAJLIS MEDIA ofisini kwake.
Amesema kwa uzoefu wake
amekua akijionea changamoto hizo na kusema kwamba asilimia kubwa ya waajiri
kwenye shule za kiislamu wanatumia mwavuli wa dini kujinufaisha wao wenyewe na
si vinginevyo ambapo hata wengine wamekua si wa kweli katika usimamizi wa
maendeleo ya shule hizo.
Aidha,amesema kuna baadhi ya
waajiri wanadiriki kuwanyima hata misaada ya dharura walimu wanaofundisha
katika shule hizo za kiislamu pindi wanapopatwa na matatizo ya gafla katika
familia zao.
KHATWIBU MAGAYANE amesema ni
ukweli usiopingika kuwa walimu wengi wanashindwa
kuzitumikia shule zenye misingi ya dini ya kiislamu kutokana na hali ya unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya
waajiri kwenye shule hizo ambapo amewataka walimu na wadau wengine wa masuala
ya elimu katika shule hizo mkoani hapa kuungana
kwa pamoja kukemea vikali vitendo hivyo ili shule hizo ziweze kuwa katika
mikono salama ya kitaaluma.
Ametaja sababu nyengine kuwa
ni baadhi ya wazazi kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa walimu huku baadhi ya
wanafunzi mkoani Tanga wakitajwa kutokua na utayari wakusoma kwa bidii ambapo
wengi wao huendekeza vitendo vya anasa mashuleni na kusema endapo changamoto
hizo zitafanyiwa kazi kwa wakati huenda suala la taalumu katika shule zenye
misingi ya dini ya kiislamu mkoani hapa likarejea katika ubora wake.
Post a Comment