Serikali kujenga kituo cha uhamiaji cha kisasa Kirongwe
Serikali imeahidi kujenga jengo la uhamiaji katika Mpaka wa Kirongwe Wilaya ya Rorya mkoani Mara ambao unatenganisha nchi za Tanzania na Kenya huku ikisema kamwe haitawavumilia watakaotaka kutumia mpaka huo kuharibu amani ya Tanzania.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mkoani Mara ambako anaendelea na ziara yake ya kikazi.
Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, waziri mkuu amesema, Kituo cha Uhamiaji Kirongwe ni kituo muhimu kwa uchumi na ulinzi wa Taifa ingawa ameshangazwa na kituo hicho kwa muda mrefu kukosa hadhi kama kilivyo Kituo cha upande wa nchini Kenya.
Waziri mkuu, anayeendelea na ziara yake mkoani Mara, amelazimika kutembelea eneo la Bubombi kilomita chake kutoka katika kituo hicho na kukutana la maombi ya wananchi wa eneo hilo waliomsihi kutaka jengo lenye hadhi linalofanana na Taifa la Tanzania.
Kuhusu vitendo vya uvamizi wa ndani katika baadhi ya maeneo ya uvuvi kwenye Ziwa Victoria, Waziri Mkuu Majaliwa amesema msimamo wa serikali ni kuhakikisha wananchi wa wilaya hiyo wanafanya shughuli zao za kiuchumi kwa kuzingatia sheria na wanajiepusha na biashara za magendo.
Waziri Mkuu amesema magendo yanaikosesha Serikali mapato, hivyo bidhaa yoyote itakayokamatwa ikiingizwa nchini kwa njia za magendo itataifishwa pamoja na chombo cha usafiri kilichotumika.
Katika hatua nyingine waziri mkuu ametembelea shule ya Sekondari ya Wasichana ya Borega, ambapo amewasisiza wananchi wasimamie elimu ya watoto wa kike ili wafikie malengo yao.
Amesema Serikali imeweka sheria kali kwa yeyote atakayekatisha masomo kwa watoto wa kike iwe kwa kumpa ujauzito au kumoa, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wanafunzi hao wasome kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kamwe wasijihusishe katika mambo ambayo hayahusiani na masomo.
Post a Comment