Tanzania Rwanda kujenga Reli ya kisasa (Standard Gauge)
Rais wa
Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame leo tarehe 14 Januari, 2018 amefanya ziara
ya kikazi ya siku moja hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Mhe. Rais Kagame amewasili katika
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na
kupokelewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na kisha kulakiwa na viongozi
mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, na baadaye
akaelekea Ikulu ambako pamoja na kufanya mazungumzo ya faragha, viongozi hao
wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika mazungumzo yao
wamekubaliana ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kati ya
Isaka nchini Tanzania na Kigali nchini Rwanda yenye urefu wa takribani kilometa
400 uanze mwaka huu (2018), na wamewaagiza Mawaziri wanaohusika na miundombinu
kukutana ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanza sasa ili kuweka mipango ya
utekelezaji ikiwemo upatikanaji wa fedha.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa
wakati uamuzi huo ukifikiwa, Tanzania ambayo tayari imeanza ujenzi wa reli ya
kati (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam – Morogoro hadi Dodoma yenye urefu
wa kilometa 726 na itakayogharimu Shilingi Trilioni 7.6, itaanza mchakato wa
kuunganisha sehemu iliyobaki ya kutoka Dodoma – Isaka yenye urefu wa takribani
kilometa 400 ili mizigo iweze kusafirishwa moja kwa moja kutoka bandari ya Dar
es Salaam hadi Kigali nchini Rwanda.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa
japo kuwa kumekuwa na ongezeko la mizigo ya Rwanda inayosafirishwa kupitia
Tanzania iliyofikia tani 950,000 kwa mwaka, biashara kati ya nchi hizi mbili sio
ya kuridhisha na hivyo amesema wamekubaliana kuboresha zaidi mazingira ya
biashara ikiwemo kuimarisha miundombinu ya reli na barabara na kuwahamasisha
wafanyabiashara wa Tanzania na Rwanda kufanya biashara zaidi.
“Tukijenga reli
kutoka Isaka hadi Kigali, na sisi huku tunajenga kutoka Dar es Salaam hadi
Dodoma na tukaunganisha Dodoma hadi Isaka, mizigo mingi ya Rwanda itasa×rishwa
kupitia bandari ya Dar es Salaam, biashara itakua zaidi na ajira zitaongezeka,
kule Lulenge Ngara, Burundi na Rwanda kote kuna madini ya Nickel, tukijenga
miundombinu yetu tutasafirisha madini haya na tutaongeza biashara.
“Na reli hii
itatumiwa na nchi nyingine za Burundi, DRC na Uganda, kwa hiyo ni jambo muhimu
sana kwa uchumi wetu na majirani” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli. Mhe. Rais
Magufuli amemhakikishia Mhe. Rais Kagame kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza
zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Rwanda kwa manufaa ya wananchi, na kwamba
ipo tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika
(AU) katika kikao cha wakuu wa nchi na Serikali kinachotarajiwa kufanyika
mwishoni mwa mwezi huu wa Januari, 2018 Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
“Mhe. Rais Kagame nakupongeza sana, unafanya kazi kubwa ya kuwapigania wananchi
wako, Watanzania tunajua ulikoitoa Rwanda na tunajua ulipoifikisha,
nakuhakikishia tutaendelea kushirikiana katika jukumu la kuwaletea wananchi
maendeleo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Rais Kagame
amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amempongeza kwa kazi nzuri
inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya
nchi yake na Tanzania.
Mhe. Rais Kagame amesema yeye na Mhe. Rais Magufuli wameamua kufanya
kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa
ushirikiano na Mhe. Rais Magufuli ili mipango yote waliyojiwekea itekelezwe
ikiwemo kuinua biashara na kuongeza ajira, na pia ameshukuru kwa Tanzania kuwa
tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa AU.
Mhe. Rais Kagame
amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini
kwake Rwanda.
Post a Comment