Tanzania yaunga mkono Umoja wa Afrika
Viongozi mbalimbali wa bara la
Afrika na Umoja wa Mataifa wamekemea vikali kauli iliyotolewa na Rais wa
Marekani, Donald Trump kuhusu mataifa ya Afrika, Haiti na El Salvador alipokuwa
katika kikao na wabunge wa nchi hiyo kilichofanyika White House.
Katika
kikao hicho, Rais Trump alishangaa Marekani kupokea wahamiaji kutoka katika
nchi hizo huku akitumia neno ‘shithole’ (tundu la choo) akimaanisha ni nchi za
Afrika Haiti na El Salvador na kwamba Marekani haihitaji wahamiaji kutoka
katika nchi hizo, badala yake inataka wahamiaji kutoka Norway.
Kufuatia
kauli hiyo, serikali ya Tanzania imetoa msimamo wake na kueleza kwamba inaunga
mkono maazimio ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mtaifa kwani ni moja wapo wa nchi
wanachama wanaounda jumuiya hizo za kimataifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amesema kwamba
kauli ya Tanzania juu ya Rais Trump imewakilishwa vizuri na Umoja wa Mataifa
(UN) na Umoja wa Afrika (AU). UN imeeleza kwamba, hakuna namna nyingine ya
kuelezea kauli iliyotolewa na Rais Trump zaidi ya ubaguzi wa rangi huku AU nayo
ikisema kauli hiyo ni ya kibaguzi.
Kwa
upande wake Rais Trump, amekanusha kutumia neno hilo na kuzihusisha na nchi za
Afrika, Haiti na El Salvador huku akikiri kwamba alitumia lugha nzito lakini
siyo tusi hilo (shithole).
Botswana ndio taifa la kwanza
Afrika kuzungumzia kauli hiyo ya Rais Trump ambapo serikali ilimuita Balozi wa
Marekani nchini humo na kutaka aeleze kama Botswana ni miongoni mwa nchi
alizozitusi Rais Trump.
Idara ya Mambo ya Nje ya Chama
cha ACT Wazalendo imesema kuwa, kauli ya Rais Trump iwe ni kengele ya kuwaamsha
viongozi wa kiafrika waweze kuhakikisha wanajitegemea kiuchumi na kutokomeza
umasikini.
Post a Comment