Viongozi watakiwa kutoa taarifa za fedha za miradi kwa wananchi

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza mawaziri wote, naibu Mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya na wakurugenzi watoe taarifa za fedha za miradi ya maendeleo kwa wananchi badala ya kusubiri ziara za viongozi wakuu.

Ametoa agizo hilo ,Januari 6, wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwenye kikao kilichofanyika katika hoteli ya Mt. Vicent, mjini Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

Waziri mkuu amesema .Kuanzia sasa ninaagiza, viongozi wote wa ngazi za juu wakiwemo mawaziri hadi wakurugenzi na hata ninyi wakuu wa idara mnawajibika kutoa taarifa za fedha tunazopeleka kwenye miradi kwa sababu wananchi wana haki ya kujua utekelezaji wa ahadi za Serikali, 

“Mnapopata fursa ya kupanda jukwaani, tumieni wasaa huo kueleza kazi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali. Elezeni Serikali imeleta fedha kiasi gani, kwa ajili ya kitu gani na kwa kufanya hivyo, mtasaidia kutoa taarifa za utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na mheshimiwa rais Dkt. John Magufuli wakati wa kampeni,” amesema.

Amesema wananchi wana haki ya kupatiwa taarifa za utendaji wa Serikali yao na kuwataka viongozi hao wasisubiri ziara za viongozi wa kitaifa. “Nendeni mkaongee na wananchi, msiwaachie wakuu wa wilaya au wabunge peke yao ndiyo waseme na wananchi,” alisema.
Waziri mkuu leo anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kukagua kituo cha kufua umeme kilichopo Unangwa, kuweka jiwe la msingi la ofisi ya TANESCO, kuzungumza na wananchi na kisha kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Songea.

No comments