Serikali yatoa msimamo kuhusu fedha za kigeni
Serikali
haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini bali imechukua hatua ya kudhibiti
matumizi ya fedha hizo ili kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Hayo
yalielezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
alipokutana na wawakilishi wa wafanyabiashara mkoani Arusha kujadiliana mambo
mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya biashara nchini.
Amesema
kuwa sheria haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini lakini inasisitiza
kuwa watu wanapaswa kutambua kuwa sarafu ndiyo fedha halali kwa malipo ndani ya
nchi. “Tatizo kubwa tunalokumbana nalo
ni uhuru ulioachiwa ambao unasababisha kushuka kwa thamani ya Shilingi yetu
kwani kila mmoja anaweza kutumia fedha za kigeni pia watumiaji wa fedha za
kigeni hawafuati thamani ya fedha iliyoko sokoni kila mmoja anakuwa na kiwango
tofauti cha thamani ya kubadili fedha za kigeni”.
Alifafanua
Dkt. Kijaji. Ili kuondoa changamoto hizo Serikali imeamua kurekebisha sheria ya
matumizi ya fedha za kigeni na sheria ya Benki Kuu huku ambayo inazitaka bei
zote hapa nchini zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania.
Bei
hizi zinajumuisha kodi za nyumba za kuishi na ofisi, bei za ardhi, gharama za
elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki. “Bei
ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja ambao sio wakazi zinaweza
kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za
kigeni.
Hata
hivyo kama mlengwa akitaka kulipa kwa Shilingi ya Tanzania asilazimishwe kulipa
kwa fedha za kigeni” alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha,
viwango vya kubadilishia fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika
sarafu nyingine vimetakiwa kuwekwa wazi na visizidi vile vya sokoni.
Mkazi yeyote wa Tanzania au mtu wa nje
anayeishi Tanzania asilazimishwe kufanya malipo yoyote kwa kutumia fedha za
kigeni kama ana Shilingi ya Tanzania mkononi mfano gharama za shule na hoteli.
Aidha
Serikali imeagiza vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote
watakaokiuka maagizo hayo yaliyotolewa na Serikali.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji alitoa rai kwa
wafanyabiashara nchini kuhimiza matumizi ya sarafu ili kuweza kukuza thamani ya
Shilingi hivyo kusaidia kuinua uchumi wa nchi.
Post a Comment